Kyelafm Radio

Sauti yako mafanikio yako

Ndugai asema hatima ya CAG, Halima Mdee kujulikana mkutano ujao wa Bunge

Dodoma. Bunge limemaliza vikao vyake jijini Dodoma leo
Jumamosi Februari 9, 2019 huku Spika, Job Ndugai akisogeza
mbele kueleza taarifa za kuhojiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mbunge wa
Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Januari 21, 2019 Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge ilimhoji Profesa Assad aliyeitwa mbele ya kamati hiyo
kueleza kauli yake kuhusu “udhaifu wa Bunge.”
Profesa Assad aliitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli
aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha
Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York,
Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.
Alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za
kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha
ufisadi.
Mbali na Assad, Januari 22 kamati hiyo ilimhoji Mdee ambaye
aliunga mkono kauli ya CAG kuhusu Bunge.
Akizungumza bungeni leo, Ndugai amesema taarifa za kamati hiyo
ziko tayari lakini muda haukutosha kuzisoma hivyo zitasomwa
Bunge lijalo.
“Waheshimiwa wabunge taarifa za kamati ya maadili ziko tayari
lakini tunakosa muda kama mnavyoona wenyewe, tutazileta
katika mkutano ujao,” amesema Ndugai
Amesema hana pingamizi na Bunge kukosolewa lakini si kwa
kushambulia kama wanavyofanya wengine.
“Tushauriane, tusaidiane lakini tusidharauliane, haiwezekani mtu
mmoja kutoka nje na kushambulia Bunge, sisi sote hapa ni watu
wazima na tumechaguliwa na Watanzania,” amesema.